Sunday, September 19, 2010

KASHOGI JUMA NA JUMA SHABANI VIJANA WAWILI WANAOSHINDA JALALANI KUTAFUTA RIZIKI YAO


HAPA NI JALALANI MAHALA AMBAPO VIJANA HAWA WAWILI (KASHOGI JUMA NA JUMA SHABANI) WANAPO LALA MARA BAADA YA KUMALIZA SHUGHULI YAO.


KASHOGI JUMA NA JUMA SHABANI WAKIWA KAZINI JALALANI



Nikiwa mkoani Mbeya niliamua kwenda kutembelea eneo la kuhifadhia taka maarufu kama dampo lilipo eneo la Uyole-Nsalaga mkoani Mbeya.
Nikiwa katika dampo hilo hilo nakutana na vijana wawili Kashogi Juma mwenye umri wa miaka 38 na mwenzie Juma shabani mwenye umri wa miaka 21. Vijana hawa wanaendesha maisha yao kutokana na kile wanachopata kutoka katika dampo hili.
Kashogi na Juma ni wakazi wa Dar es Salaam eneo la Manzese Uzuri na hapa Mbeya katika dampo hili wamekuja kufanya kazi ya kukusanya vyupa chakavu na kuvipasuapasua katika vipande vidogovidogo tayari kusafirishwa kwenda jijini Dar es Salaam kwa mauzo. Nilipo wauliza kwa nini kazi hii wasinge ifanya hapo hapo Dar es Salaam ama mikoa ya karibu kama Morogoro? Walinijibu kuwa Dar es Salaam na Morogoro tayari kumevamiwa na vijana kama wao ambao wanafanya kazi kama hii.
Cha kushangaza vijana hawa wanalala hapahapa Dampo kama picha inavyo onyesha. Vijana hawa wako hatarini kupata magonjwa yanayo sababishwa na uchafu kwa kuwa eneo hili lina harufu kali ya vitu vilivyo oza.
Vijana hawa huuza shilingi 80,000 kwa kila tani moja ya vyupa chakavu na shilingi 200,000 kwa kila tani moja ya Vyuma chakavu.
Vifurushi hivi husafirishwa kwenda Dar es Salaam kwa ajili ya mauzo. Je kuna vijana wangapi wanaweza kuvumilia kufanya kazi kama hii kabla hawajafikiria kuwa wezi na majambazi ili kujipatia kipato. Maisha bora kwa kila mtanzania yako wapi?

RIZIKI YA Bi ZAINAB MOHAMED KATIKA DAMPO LA NSAGALA UYOLE, MBEYA



Pia katika Dampo hili Nsagala-Uyole Mbeya, nilikutana na Bi, Zainab Mohamed mjane mwenye umri wa miaka 45 na watoto wanne. Mama huyu anakusanya chupa katika mifuko midogo midogo na kuuza mfuko mmoja kwa shilingi 300.
Bi, Zainab alipo ulizwa ni mtaji kiasi gani anahitaji ili aweze kufanya biashara ambayo si hatarishi kwa afya yake, Bi, Zainab alisema kuwa shilling 50,000 itamtosha kufungua biashara ambayo haitakuwa hatarishi kwake.
Mama huyu anaingia katika dampo hili kila siku kuanzia saa 12 asubuhi na kutoka saa moja jioni.

Saturday, September 18, 2010

KIJANA MUSA MARTINI KATIKA DAMPO LA UYOLE-NSAGALA MKOANI MBEYA


Pia katika Dampo hili la Uyole-Nsagala, nilikutana na kijana mwingine anayeitwa Musa Martini, yatima mwenye umri wa miaka 17, Kijana huyu ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari ya Uyole day. Yupo katika dampo hili kutafuta makopo ambayo atayatumia kutengeneza vibatari ambapo kila kimoja huuzwa kwa shilingi 150. Nilipo muuliza kwa nini haendi shule na badala yake yupo kwenye dampo hili kukusanya makopo hayo, alinijibu kuwa shuleni anadaiwa ada ya shilingi 15,000 baada ya kulipa shilingi 5,000 kama ada ya mwaka katika shule hiyo. Ada yake ya mwaka ni shilingi 20,000. Musa Martini hulazimika kukatisha masomo yake kwa baadhi ya siku na kuja katika dampo hili kukusanya makopo na kutengeneza vibatari ili kupata ada ya shule. Musa Martini anaishi na mdogo wake ambaye yeye hakupata bahati kufaulu na kuendelea na masomo.
Fikiri kijana Musa Martini atakusanya makopo mangapi na atengeneze vibatari vingapi atakavyo viuza apate ada ya shule pamoja na hela ya kupata mahitaji mengine ya kibinadamu. Kumbuka kibatari kimoja kinauzwa shilingi 150, na je ni vibatari vingapi vitanunuliwa ili apate kuishi? Huyu ndiye mtanzania wa taifa la kesho.

KIJANA ERICK JACKSON KATIKA DAMPO LA UYOLE-NSAGALA MKOANI MBEYA



Eric Jackson ni kijana mdogo mwenye umri wa miaka 15. Kijana Erick Jackson anaendesha maisha yake ya kila siku kwa kutafuta chuma chakavu katika dampo hili lenye harufu kali na uchafu wa kila aina.
Maisha ya kijana huyu yanaonyesha wazi kua ni magumu kwa binadamu wa kawaida kuishi. Anachokifanya kijana huyu katika dampo hili ni kukusanya vyuma chakavu na baadaye kwenda kuviuza kwa wachuuzi wengine. Erick Jackson anauza vyuma chakavu vyenye uzito wa kilogramu kumi kwa shilingi 1,500.
Inamchukuwa siku nzima kushinda katika dampo hilo ili kupata kilo 10 za vyuma chakavu.
Mtoto Erick Jackson anatumia jembe na mikono yake ambayo haina kinga yeyote kufukua mlundikano wa takataka ili kupata chuma chakavu. Wakati mwingine itamchukua siku mbili mpaka tatu kupata kilo kumi za chuma chakavu. Kwa mantiki hiyo mototo Erick Jackson anatafuta shilingi 500 kwa siku kwa ajili ya kujikimu maisha yake. Je, Mahitaji muhimu ya mwanadamu ambayo ni chakula, malazi na mavazi anayatimiza kwa kiwango gani kama pato lake ni shilingi 500 kwa siku? Maisha ya mtanzania pamoja na kuwa ni umasikini lakini vilevile ni hatari.

Friday, September 3, 2010

UHABA WA HUDUMA YA MAJI SAFI NA SALAMA, CHANZO CHA UCHAFUZI WA MAZINGIRA KATIKA MWALO WA KAYENZE - MAGU MWANZA




Huu ni mwalo ulioko KAYENZE, MAGU mkoani Mwanza. Mwalo huu unatumika kwa shughuli nyingi kama inavyoonekana katika picha hizi. Wakazi hawa wangepata huduma ya maji safi na salama huu Mwalo ungebaki salama na pengine magonjwa ya milipuko kama Kipindupindu, kichocho, na mengineyo yangepungua ama kuisha kabisa.

USIKAE HAPA


Je tuamini kuwa aliyevunja maagizo haya hakuelewa lugha ya Kiswahili ama ni tabia tu ya walio wengi kupuuza maagizo...

Thursday, September 2, 2010

UFADHILI KUTOKA MOIL




Ni faraja iliyoje kwa chama cha mpira wa kikapu mkoani Mwanza MRBA kupata ufadhili wa Trak Suit 30 kutoka kwa kampuni ya ununuzi na usambazaji wa mafuta MOIL iliyo jijini Mwanza. Wadau hawa wamekuwa mstari wa mbele kuhakikisha mchezo wa mpira wa kikapu unakuwa kwa kutoa misaada mbalimbali. Hivi karibuni timu ya mpira wa kikapu mkoani Mwanza ilisafirishwa na kampuni hii ya MOIL kuelekea Bulyanhulu kwa ajili ya mechi ya kirafiki.

TUZO ZA WAANDISHI WALIOFANYA VIZURI KATIKA UANDISHI WA HABARI ZA MAZINGIRA ZIWA VICTORIA.


Lake Victoria Environment Management Project (LVEMP) hivi karibuni waliandaa mashindano ya muandishi bora wa habari za mazingira katika ukanda wa Ziwa Victoria. Pichani ni waandishi wa habari waliofanya vizuri katika zoezi hilo.
Kutoka kushoto ni Bw. Deus Bugaywa kutoka gazeti la The Guardian, Katikati ni Bw. Vedastus Msungu kutoka ITV/Radio One na Kulia ni Bi. Diana Nachilonga kutoka Gazeti la Mwananchi. Hongereni