Monday, November 16, 2009

Wakufunzi, Wahariri wa habari msiache kuandika

Na Victor Maleko

Wahariri wa vyombo vya habari na Wakufunzi wanaofundisha kwenye tasnia ya habari nchini wamehimizwa kuwa mfano wa kuigwa kutoa elimu ya habari kwa njia ya kuandika habari, fursa itakayowafanya waoneshe umahiri wao kwa wanafunzi wanaowafundisha.

Changamoto hiyo ilitolewa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Bw. Kajubi Mukajanga kwenye mafunzo yaliyoandaliwa kwa ajili ya Wakufunzi wa tasnia ya habari, yaliyofanyika Jijini Mwanza hivi karibuni.


BAADHI YA WAKUFUNZI WAKIJADILI JAMBO KATIKA MAFUNZO HAYO

Bw. Kajubi ambaye alikuwa mmoja wa wawezeshaji wawili wa mafunzo hayo ya siku mbili alisema, Wahariri na Wakufunzi wa tasnia ya habari hawawezi kuwa na ujasiri wa kuyakosoa mapungufu ya habari zinazoandikwa na waandishi wao kama hawaandiki kila mara.
"Siku hizi, Wahariri wa vyombo vya habari na Walimu wa fani ya uandishi wa habari hamuandiki kabisa! Sasa mnapata wapi ujasiri wa kutambua kisha kuhariri upungufu wa habari zinazoandikwa na Waandishi wengine?!" alishangaa Bw. Mukajanga.

Aliwaambia jumla ya washiriki 11 wa mafunzo hayo kwamba kutoandika habari za kawaida na makala katika magazeti kunahatarisha ukuaji wa tasnia ya habari kwa sababu viongozi wanaotarajiwa kuonesha mfano na umahiri wa kuandika hawatimizi wajibu wao.

Akizungumzia maandalizi ya baadhi ya wanafunzi kuwa Wahariri, Bw. Mukajanga ambaye ni Mwandishi mzoefu aliyewahi kumiliki gazeti, alitahadharisha kuwa, “Msijidanganye kwa kudhani kuwa mtu yeyote anaweza kujiita Mhariri pasipo kuwa na ujuzi wala uzoefu wa uandishi wa habari za kawaida na makala" .

Naye Mwezeshaji mwenza, Bw. Fili Karashani, alieleza kushangazwa kwake kuwaona baadhi ya wahitimu wa elimu ya juu katika tasnia ya habari hawawezi kuandika habari, jambo ambalo alisema, hulazimika kuwafundisha upya jinsi ya kuandika habari wahusika hao wawapo makazini.

Kwa upande wake, Mhariri wa gazeti la ‘Msanii Afrika’ na Jarida hili, Bw. Calvin Jilala alisema, uhalali wa mtu aliyepewa dhamana ya Uhariri kufanya kazi yake unatokana na uandishi bora wa habari unaomwezesha kukuza upeo wake wa kutambua usahihi, ukweli, uwazi na umakini wa hali ya juu ya mwandishi husika.

“Kimsingi Mhariri na Mkufunzi wa taaluma ya habari ni Mwandishi wa habari, hivyo si sahihi Mhariri ama Mkufunzi kuacha kazi yake kwa sababu tu kapanda daraja. Hiyo ndiyo kazi yake ya msingi. Wakumbuke wao ni viongozi wanaopaswa kuwa mfano wa kuigwa na wanaowaongoza.” Alisema Bw. Jilala.

Mafunzo hayo yaliwashirikisha Wahariri na Wakufunzi kutoka Vyuo vikuu mbalimbali vinavyofundisha elimu katika Tasnia ya habari ikiwemo Mawasiliano ya umma, uandishi wa habari na kadhalika.

No comments:

Post a Comment